. Atuhumiwa kumnywesha sumu mwandishi
. Ana siri nzito ya ufisadi anaoufanya
. Daktari athibitisha kuwa alinyweshwa sumu
. Polisi makao makuu wakiri kupokea madai
. Ana siri nzito ya ufisadi anaoufanya
. Daktari athibitisha kuwa alinyweshwa sumu
. Polisi makao makuu wakiri kupokea madai
Bollen Ngetti na Iddy Mkwama
MWANDISHI wa habari wa zamani wa mmiliki wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, John Marandu amemtuhumu mfanyabiashara huyo kwa kumbambikia kesi na kumnyweshwa sumu katika mazingira ya kutatanisha.
Gazeti hili lina barua ya Agosti 29 mwaka jana yenye Kumb. Na. Pf.03/Pol/29/08 na nyaraka zote juu ya sakata hilo ambazo zilipelekwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba kuomba jeshi hilo kuingilia kati upelelezi wa kesi yake.
Katika barua hiyo Marandu ambaye aliachishwa kazi na Mengi, alisema alikamatwa na askari wa kituo cha Osterbay akidaiwa kuwa na fomu za maombi ya hati ya kusafiria ya Tanzania ya Mama mkwe wa Mengi Caritas Paulsen.
Caritas ni mama wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni maarufu ya Benchmark Productions, Rita Paulsen anayedaiwa kuwa mke mdogo wa Mengi.
Barua hiyo ya Marandu inadai kuwa, Caritas si raia wa Tanzania, bali anatoka katika kabila la Wanyamulenge wa nchini DRC.
Inaendelea kusema kuwa, walifuatilia hatua kwa hatua fomu hizo hadi uhamiaji ingawa mara kadhaa kulionekana kuna utata na kutakiwa kuzirudisha kwa wahusika ili kujazwa upya.
Fomu ambazo zilikosewa ndio ambazo Marandu alikua nazo, moja aliiweka ofisini kwake na nyingine aliipeleka nyumbani kwake alipokuwa akiishi maeneo ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Marandu anadai kuwa zoezi la kupatikana kwa hati hiyo lilikamilika na kutolewa ingawa katika hatua za mwisho hakushirikishwa na hajui ilitolewa kwa utaratibu gani na timu ya uchunguzi wa gazeti hili linaendelea kufuatilia kwa makini mchezo mchafu unaodaiwa kufanyika katika kupatikana kwa hati hiyo.
Inadaiwa kwamba, siku chache baada ya kupatikana kwa hati hiyo, Marandu na mfanyakazi mwenzake (jina tunalo) walikaa kwenye baa moja inayoitwa Bamaga maeneo ya Sinza, ambapo Marandu alimlalamikia mwandishi huyo kufanyishwa kazi za nje ya taaluma yake ikiwemo kughushi hati hiyo.
“Nina wasiwasi, huenda mfanyakazi huyo alikwenda kunisaliti kwamba namlalamikia Bw. Mengi, kwani siku chache kiongozi wangu huyo, alianza kuwa mkali kwangu wakati mwingine kunitukana na kunifokea bila sababu”.
“Hatimaye kufuatiwa na kitendo cha kuvunjwa kwa droo ya meza ya ofisini kwangu ambako ile fomu ya kwanza ya maombi ya hati ya kusafiria iliyokuwa na jina la CARITAS PAULSEN ilichukuliwa na mtu nisiyemfahamu” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Siku chache baadaye, Marandu alipata ajali ya gari na kulazwa katika Hospitali ya Muhimbili na baada ya kupona Mengi alimhamisha kutoka ofisini kwake na kumpeleka ITV na baada ya kuripoti alipewa uhamisho mwingine wa kwenda Arusha.
“Arusha wakati ule hakukuwa na ofisi. Nilifanya kazi katika mazingira magumu kwa muda wa miaka mitano, kiasi cha kulazimika kutumia fedha zangu mwenyewe ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa ya mshahara wangu kwa kufanya kazi za kampuni”
Aidha kwa mujibu wa kumbukumbu ambazo Marandu anazo, zinaonyesha kuwa alitumia kiasi cha Shilingi 18, 732,000.00
“Ilipofika mwaka 2002, nilikata tamaa nikitaka kuacha kazi. Nikaandika barua kudai nilipwe fedha hizo na pia ikibidi nirudishwe Dar es Salaam kikazi maana nilijiona ni kama ninayetumikia adhabu maalum kule, niliathirika vibaya kisaikolojia na hata kiafya kutokana na mateso na manyanyaso niliyokuwa nikipata kutoka kwa mwajiri wangu”
“Nilijaribu mara nyingi kuomba kukutana na Bw. Mengi nimsimulie matatizo hayo, lakini alinikwepa na hatimaye nikawa nasikia kutoka kwa wafanyakazi wenzangu, kwamba Mengi alikuwa akisema ‘huyo ni mgonjwa mwacheni aji-face out mwenyewe polepole” ilidai barua hiyo.
Aidha katika barua hiyo, Marandu aliendelea kusema kuwa: “Nasikitika sana kwamba kufuatia barua ya kuacha kazi, kwa sababu hizo za kiafya niliyomwandikia mwajiri wangu, mwajiri huyo kwa lengo la kunidhalilisha alieneza taarifa kwa watu wengi, akidai nilikuwa na UKIMWI na kwamba ni mtu wa kufa siku yoyote.
Huo pia ulikuwa ni unyanyasaji mbaya usiozingatia maadili na haki za kibinadamu pamoja na utunzaji wa siri ya afya ya mtumishi hata kama ameachishwa, ameacha amestaafu au amefukuzwa kazi”
Hata hivyo, miezi michache kabla hajaomba kuacha kazi, ITV ilifungua ofisi katika kituo cha mikutano cha AICC na kukabidhiwa Ayubu Semvua ambapo baada ya kukabidhiana ofisi, Marandu aliomba kupatiwa mafao yake kwanza, lakini katika mabishano makali, Semvua alimpeleka kituo cha polisi mjini Arusha lakini OCD wake alitupilia mbali malalamiko hayo.
“Tuliporejea ofisini, Semvua aliniambia kwamba Mengi alikuwa tayari kunilipa haki zangu pamoja na madai mengine niliyokuwa nayo, ili mradi nikubali kuwapatia nyaraka nilizokuwa nazo kuhusu maombi ya uraia wa mama yake Rita Paulsen” alisema Marandu kupitia barua hiyo.
Baadaye Semvua alizungumza na Mengi na kumwelekeza kwenda kiwanda cha Bonite Bottlers cha mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro na kuchukua Sh. 18, 732,00 kwa sharti la kukabidhiana nyaraka hizo.
“Siku iliyofuata Semvua alikwenda Moshi na kuniletea malipo ya Sh. 18,000,000, zikiwa ni pungufu ya 732,000, wakati ananikabidhi fedha hizo ndani ya ofisi ya benki ya Standard Chartered mjini Arusha, Semvua aliendeleza mazungumzo yake kusisitiza kupatiwa nyaraka zilizokuwa zinahitajika na Mengi, mbele ya yule afisa wa benki”
“Baada ya hapo aliniomba nimpatie kamisheni ya shilingi 1,000,000, mbele ya afisa huyo wa benki, kabla hatujapanda gari dogo kutoka pale benki, huku akiendelea kusisitiza kuhusu Bw. Mengi anavyokosa raha asipopata documents hizo mbili. Nilimuomba yule dereva wa gari aliyekuwa akituendesha, kusikiliza kwa makini mazungumzo yote ya Bw. Semvua kuhusu hati hizo”
Barua hiyo iliendelea kusema kuwa, Marandu alimpeleka Semvua sehemu inapochomwa nyama, ambako waliwekwa mashahidi kabla hajaondoka, kwa makubaliano kwamba kesho yake apelekewe hizo ‘documents’ ili Mengi asije kumuona tapeli.
“Siku iliyofuata Semvua alipiga simu kupitia simu ya yule shahidi aliyekuwa akituendesha na gari yake, akiomba apelekewe zile documents lakini nilimkatalia sikuwa tayari kufanya hivyo hadi nitakapomaliziwa madai yangu”
Marandu katika barua yake hiyo alisema baada ya kusikia hivyo Semvua aliondoka na kurejea Dar es Salaam, huku akimtisha kwamba alikuwa akicheza na ‘a powerful figure.’
Maneno hayo hayakumtisha Marandu, aliandika barua ya madai ambayo hayakujibiwa hivyo akaamua kwenda Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta msaada wa kisheria.
Alisema wakati akiwa jijini, maeneo ya Shekilango Hotel, walimjia watu wawili waliojitambulisha kama Nyanda na Ngaiza ambao walimuomba wampatie nakala ya ‘demand note’ madai yake ili wamfikishie mwenyewe.
“Niliwakabidhi nakala hiyo na kesho yake waliporudi, walinieleza mbele ya ushahidi kwamba Mengi ameomba nikutane naye kwenye hotel yoyote yenye hadhi yake (Mengi) akanilipe madai yangu, ili mradi tu nikubali sharti la kumpatia documents ambazo nilikataa kumpa Semvua kule Arusha”
Marandu aliendelea na msimamo wake wa kukataa ombi hilo na kuwaambia kwamba kama Mengi ni mtu mwema, amlipe mbele ya wanasheria tena bila masharti yoyote, kwa kuwa fedha hizo ni jasho lake.
Mwandishi huyo aliendelea kusema kuwa, siku iliyofuata asubuhi maafisa wawili wa polisi kutoka kituo cha polisi Osterbay walifika na kuchukua hati ya pili ya uhamiaji na kumfungulia jalada la uchunguzi namba P.E 59/2008.
Madai yaliyoandikwa kwenye jalada hilo ni kwamba, Marandu anajihusisha na shughuli za kitapeli za kuwatafutia hati za kusafiria watu wasio raia wa Tanzania.
Anasema baadaye aliachiwa huru baada ya kudhaminiwa ingawa ilimbidi kukaa kituoni hapo kumsubiri askari ambaye alitakiwa kuonana naye na alijaribu kumtafuta kwa simu yake ya mkononi lakini hakuwa anapatikana.
“Wakati nikiendelea kusubiri kituoni pale, alijitokeza mtu mmoja aliyejifanya rafiki na baada ya kuzungumza naye kwa muda mrefu, mtu huyo ambaye simfahamu kwa jina, alinitaka twende kantini ya polisi ambako alininunulia soda”
“Baada ya kunywa kiasi kidogo tu soda ile, nilianza kupata maumivu ya kichwa, kizunguzungu, kutapika, kuharisha mfulululizo, kuishiwa nguvu mwilini na hatimaye kuanza kupoteza fahamu, hadi nilipolazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili”
Madaktari wa Muhimbili walifanikiwa kuokoa maisha yake na kubainisha kuwa alikunywa soda iliyowekwa sumu au madawa ya kulevya kwa lengo la kumdhuru na hata kwenye cheti chake Na. A 309104 kinaonyesha hivyo.
Katika barua hiyo, Marandu aliomba jeshi la polisi kwa kutumia maafisa wake waadilifu kutoka makao makuu kuchunguza suala hilo ili ukweli ufahamike na kutaja watu anaotaka wahojiwe.
Mtu wa karibu wa Marandu ambaye gazeti hili lilifanikiwa kuhojiana naye anadai kwamba, Marandu mara zote alikuwa anasisitiza kuwa anahisi kuna hujuma anataka kufanyiwa kwa kuwa amekataa kutoa nyaraka hizo na kufahamu mambo mengi mazito yanayomuhusu mfanyabiashara huyo.
Waandishi wa habari wa gazeti hili kwa kupitia vyanzo vyake, kwa wiki ya kwanza walipoanza kufuatilia suala hili, walifanikiwa kupata namba ya simu ya askari aliyepewa jukumu la kufuatilia kesi hiyo ACP Ubisi Mbali lakini alipopigiwa alikana kutojua kesi hiyo.
Baadaye Sauti Huru katika uchunguzi wake uliochukua takribani wiki tatu, ulifika Makao makuu ya polisi hadi kitengo kinachohusika na malalamiko ya raia na askari ambapo msemaji wa kitengo hicho MM. Gyumi hakuwa tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kukamilisha uchunguzi huu.
Baadaye askari mmoja aliyekuwa ndani ya ofisi ya Gyumi baada ya kuona hakuna mwafaka wa kupatiwa ufumbuzi suala hili kwenye ofisi hiyo, aliwaongoza waandishi hadi kwenye ofisi ya IGP ambapo licha ya juhudi za kutafuta nakala ya barua iliyotumwa na Marandu haikupatikana na kuelekezwa ikatafutwe kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba.
Katika masijala ya siri ya DCI barua hiyo pia haikupatikana ingawa muhusika wake alikiri kuiona kwa siku za nyuma na kuelekeza iende kutafutwa kwenye masijala mengine na ndipo barua hiyo ilikutwa na kuelekezwa mtu ambaye anashughulikia madai hayo ambaye ni yule yule ACP Ubisi “aliyeruka”, na wahusika kuelekeza ilipo ofisi yake maeneo ya Kamata jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo ya uchunguzi ya gazeti hili ilifika kwenye ofisi ya Ubisi na kujibiwa kuwa ametoka na hakuna uhakika wa kurudi na kupewa namba yake ya simu ya mkononi ambayo ilifanana na ile aliyopigiwa siku ya kwanza na kukana.
Alipopigiwa Ubisi kwa mara nyingine na mwandishi kujitambulisha alijibu kwa ukali: “nyie mnafanya kazi kwenye simu tu. Hamji ofisini,” hata baada ya kuambiwa waandishi walifika ofisini kwake mara mbili aliuliza: “ofisi yangu ipo wapi? Alipojibiwa Kamata akasema: “mimi sipo huko, ofisi yangu ipo makao makuu”
ACP Ubisi aliendelea kuzungumza kwa ukali na kisha akasema:“unapaswa kuja makao makuu kufuatailia suala hilo” na hata alipoambiwa kote waandishi wamepita akasema “jalada nimeshalipeleka kwa DPP, nitafuteni Jumatatu” na kisha kukata simu.
Hata hivyo bado gazeti hili linaendelea kufuatilia sakata hilo ingawa upande wa pili wa Mengi hakuna aliyetoa ushirikiano, simu yake mara zote ilipopigwa iliita bila kupokelewa, sektretari wake naye hakuwa tayari kupokea na msemaji wake Abdulhamin Njovu hakuwa anapatikana na hata alipoachiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu ingawa badaaye ulionyesha kupokelewa na hadi tunakwenda mitamboni hakuna jibu lolote lililopatikana.
Jitihada za kumpata mlalamikaji (Marandu) ili kujua kinachoendelea kwa upande wake zimegonga mwamba kwa wiki ya pili sasa kwani hata watu wake wa karibu wanaomfahamu hawajui alipo na simu yake ya mkononi haipatikani.
“Tumejaribu kumtafuta kwa muda mrefu sasa hapatikani na wala hatujui alipo” alisema mtu huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini kwa sababu za wazi.